Kuhusu misheni ya uangalizi wa uchaguzi wa Kenya , 2022
Kufuatia mwaliko kutoka kwa serikali ya Kenya, Umoja wa Ulaya umewatuma waangalizi wa uchaguzi mkuu wa 9 Agosti 2022.
Jukumu la waangalizi hao ni kutathmini uchaguzi mkuu wa 2022 kulingana na mfumo wa kisheria wa Kenya na vile vile viwango vya kimataifa na kikanda pamoja na hatua ambazo Kenya imechukua kuhakikisha uchaguzi wa kidemokrasia.
Waangalizi hawa watatoa uchanganuzi wa kina, wa mchakato mzima wa uchaguzi, na usiopendelea upande wowote kulingana na mbinu za Umoja wa Ulaya za kuangalia uchaguzi.
Historia ya Uangalizi wa Uchaguzi wa EU
Kulingana na mbinu za kuangalia uchaguzi za Umoja wa Ulaya, waangalizi hawaruhusiwi kuingilia mchakato wa uchaguzi , kubadilisha au kurekebisha kasoro zozote. Waangalizi wote wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya wanapaswa kuzingatia kanuni na miongozo ya kimaadili ambayo inahakikisha kutoegemea na kutopendelea upande wowote.
EU EOM inafanya kazi kwa mujibu wa ‘Kanuni za Uangalizi wa Uchaguzi wa Kimataifa’ zilizoidhinishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2005, na kufikia sasa zimetiwa saini na zaidi ya mashirika 50 ya kimataifa yanayohusika na uangalizi wa uchaguzi kote duniani, likiwemo bara la Afrika.
EU EOM haihalalishi mchakato wa uchaguzi wala kuidhinisha matokeo ya uchaguzi. Jukumu lake ni kuchunguza, kukusanya na kuchambua taarifa kuhusu mchakato wa uchaguzi na kuhakikisha kuwa matokeo na hitimisho zote zinatokana na habari iliyothibitishwa kwa uangalifu.
EOM ni huru katika kutoa matokeo yake kutoka kwa Wajumbe wa EU nchini Kenya, nchi wanachama wa EU, na taasisi zote za EU.
Misheni
Misheni ya mwaka huu inaongozwa na Mwangalizi Mkuu Ivan Štefanec, Mbunge wa Bunge la Ulaya kutoka Slovakia. Kikundi kikuu kinawajumuisha wataalamu 12 wa uchaguzi ambao waliwasili mjini Nairobi tarehe 27 mwezi Juni. Tarehe 9 Julai, Waangalizi 48 wa muda mrefu watajiunga na misheni na watapiga kambi kote nchini kufuatilia mchakato wa uchaguzi katika mikoa. Baadaye, waangalizi 48 wa muda mfupi watajiunga na misheni siku ya uchaguzi kuchunguza ufunguzi, upigaji kura, kuhesabu na kujumlisha matokeo. Waangalizi wengine wa kipindi cha muda mfupi kutoka Jumuiya Ulaya pamoja na kutoka Canada, Norway na Uswizi wataimarisha misheni siku ya uchaguzi. Misheni hiyo itasalia nchini hadi mchakato wa uchaguzi utakapokamilika.
Kulingana na mpangilio wa uangalizi wa uchaguzi wa EU, misheni itatoa taarifa ya mapema na kufanya mkutano na vyombo vya habari jijini Nairobi baada ya uchaguzi.
Ripoti ya mwisho ambayo itajumlisha mapendekezo kwa michakato ya uchaguzi ya siku za usoni itawasilishwa kwa washikadau baada ya kukamilika kwa mchakato mzima wa uchaguzi.
Misheni itatathmini vipengele vyote na hatua zote za mchakato wa uchaguzi ikiwa ni pamoja na:
- mfumo wa kisheria na utekelezwaji wake
- utendaji wa usimamizi wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia mpya
- jukumu la taasisi za serikali
- uandikishaji wa wapiga kura
- shughuli za kampeni na fedha za kampeni
- mazingira ya uchaguzi kwa jumla, ikijumuisha kuheshimu uhuru wa kimsingi, haki za kiraia na kisiasa
- ushiriki wa wanawake na makundi hatarishi
- jukumu la vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na vyanzo vya habari vya mtandaoni na mitandao ya kijamii
- jukumu la asasi za kiraia
- upigaji kura, kuhesabu na kujumlisha
- mchakato wa malalamiko na rufaa
- kutangazwa kwa matokeo