Uhuru wa kimsingi uliheshimiwa katika uchaguzi mkuu wa Kenya, lakini mapungufu katika utaratibu yanaonyesha hitaji la kuboreshwa

Mwangalizi Mkuu, Bw. Ivan Štefanec, Mbunge wa Bunge la Ulaya kutoka Slovakia, aliwasilisha leo matokeo ya awali ya Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU EOM) kuhusu uchaguzi mkuu wa Agosti 9 nchini Kenya.

"Wapiga kura wa Kenya walipiga kura zao kwa subira katika ngazi sita za uchaguzi mkuu ambao uliwapa wapiga kura chaguo halisi la wagombea na haki za kimsingi ziliheshimiwa kwa ujumla katika kipindi chote cha kampeni. Mabadiliko ya dakika za mwisho katika mchakato wa uchaguzi yalionyesha kuwa vipengele vya utaratibu bado vinastahili kuboreshwa.” alisema Bw Štefanec katika kikao na wanahabari jijini Nairobi leo.

Siku ya uchaguzi, ufunguzi, upigaji kura na kuhesabu kura ulifanyika kwa ujumla kulingana na taratibu zilizowekwa, lakini hatua muhimu za uadilifu nyakati fulani hazikufuatwa, hasa katika taratibu za kuhesabu kura. EU EOM inabainisha kuwa mchakato wa kujumlisha unaendelea, na waangalizi wake watasalia nchini hadi kukamilika kwa mchakato wa uchaguzi.

Mfumo wa kisheria unatoa msingi mzuri wa kufanya uchaguzi wa kidemokrasia, lakini mengi zaidi yangefanywa ili kurekebisha sheria za uchaguzi kati ya chaguzi na pia kutekeleza vipengele vya uthibitisho wa Katiba ya mwaka 2010. Kinyang'anyiro cha urais kilikuwa na hadhi ya juu zaidi, lakini umuhimu wa kinyang'anyiro cha ugavana ulionyesha kuongezeka kwa umuhimu wa ugatuzi wa mamlaka kikatiba.

Wakati hatua za maandalizi ya uchaguzi zilisimamiwa ipasavyo na kitaalamu na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, siku ya uchaguzi ilipokaribia, hali ya sintofahamu kuhusu mambo muhimu iliendelea ambayo iliathiri taratibu za siku ya uchaguzi. Mengi ya maamuzi haya yangeweza kuzingatiwa mapema lakini badala yake yalishughulikiwa punde yalivyoibuka, wakati mwingine kutokana na kesi za muda mrefu.

"Ukosefu wa mfumo sahihi wa fedha za kampeni uliharibu mazingira ya kampeni, na kuunda uwanja usio sawa, na kuwakosesha fursa wale waliokuwa na uwezo mdogo wa kupata fedha, hasa wanawake, ambao walikuwa asilimia 12 pekee ya wagombea." Alisema Bw Štefanec.

Vyombo vya habari vilikuwa vikiripoti uchaguzi kwa upana, ingawa upendeleo katika vyombo vya habari vya matangazo ya moja kwa moja ulibainika, hasa katika redio za lugha za asili. Mitandao ya kijamii ilitumiwa sana wakati wote wa kampeni, lakini taarifa potofu zenye vipengele visivyo vya kweli pia zilienezwa kupitia majukwaa ya mtandaoni.

Bi. Evin Incir, Mkuu wa ujumbe wa Bunge la Ulaya kutoka Sweden alisema: “Uchaguzi huu mkuu hadi sasa umekuwa wa amani, na ningependa kuwapongeza Wakenya. Nimefurahishwa sana na moja ya sababu ni ukweli kwamba wakati wa kampeni hii mkazo ulikuwa zaidi katika masuala ya kijamii na kiuchumi. Hata hivyo, mchakato wa uchaguzi bado unakabiliwa na baadhi ya changamoto ambazo zinafaa kushughulikiwa ili kuongeza imani ya umma”

EU ilituma waangalizi zaidi ya 180 kutoka Nchi Wanachama wa EU pamoja na Kanada, Norway na Uswizi kwa ajili ya uchaguzi mkuu. EU EOM itasalia nchini Kenya kutathmini mchakato wa malalamiko na rufaa pamoja na uwezekano wa duru ya pili ya uchaguzi wa urais.

EU EOM inafanya kazi chini ya mamlaka tofauti kutoka kwa Wajumbe wa EU nchini Kenya na ni huru katika matokeo yake kutoka kwa Nchi Wanachama wa EU na taasisi zote za EU.

Kwa habari zaidi, tafadhali wasiliana na ofisi ya waandishi wa habari ya EU EOM Kenya 2022.

Marek Mracka, Press Officer - marek.mracka@eomkenya2022.eu;  +254 712 07 09 07

 

  

 

                   

Marek Mracka

Press Officer

marek.mracka@eomkenya2022.eu

+254 712 07 09 07