Ujumbe wa Uangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya unawasilisha Ripoti ya Mwisho, ikijumuisha Mapendekezo, kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 nchini Kenya Nairobi, 27 Oktoba 2022
Ujumbe wa Uangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU EOM) nchini Kenya uliwasilisha ripoti yake ya mwisho, ikijumuisha mapendekezo mbalimbali, kuhusu Uchaguzi Mkuu wa tarehe 9 Agosti 2022. Mwangalizi Mkuu Ivan Štefanec, Mbunge wa Bunge la Ulaya, alibainisha: “Uchaguzi uliangazia mambo mengi mazuri katika mchakato wa uchaguzi wa Kenya, kuthibitisha hali ya kidemokrasia ya Kenya; lakini tunaamini kuwa maboresho yanahitajika ili kuongeza uwazi na imani ya umma, haswa kwa kuimarisha uwezo wa IEBC kutimiza wajibu wake na kuongeza ushirikishwaji katika mchakato wa uchaguzi."
Ripoti ya mwisho ya EU EOM ina jumla ya mapendekezo 21 yanayolenga kuboresha chaguzi zijazo za Kenya. Hasa, ripoti inapendekeza mabadiliko katika mfumo wa udhibiti ili kuhakikisha vifungu vya kikatiba kuhusu usawa wa kijinsia vinatekelezwa kikamilifu na kutekeleza sheria kuhusu fedha za kampeni. Pia inataka kuboreshwa kwa teknolojia ya uchaguzi na IEBC ipewe rasilimali kwa wakati ili kutekeleza elimu ya wapiga kura mfululizo.
Ripoti hiyo ni matokeo ya uchambuzi wa kina wa uchaguzi mkuu wa Agosti 2022, unaozingatia vipengele vyote vya mchakato wa uchaguzi: mazingira ya kisiasa, jukumu la vyombo vya habari na mitandao ya kijamii katika kampeni, utendakazi wa IEBC, pamoja na kufuata sheria za kitaifa na kimataifa.
Katika hotuba yake ya kumalizia, Bw Štefanec alielezea shukrani zake kwa ushirikiano wa washikadau wa uchaguzi na EOM na kusema: “Tunatumai kwamba mapendekezo haya yatachangia mazungumzo na mashirikiano kuhusu mageuzi ya uchaguzi nchini Kenya na hivyo kuimarisha ufanikishaji kamili wa kanuni na maadili ya kimsingi ya uchaguzi wa kidemokrasia kulingana na matarajio ya watu wa Kenya.”
Ripoti ya mwisho ya EU EOM inaweza kupatikana hapa, na pia kwenye tovuti www.eomkenya2022.eu na kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter: @eueomkenya2022
###
Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:
o Silvia de Félix, silvia.defelix@eomkenya2022.eu
o Faith Wamalwa, faith.wamalwa@eomkenya2022.eu