Umoja wa Ulaya umetuma waangalizi 48 wa muda mrefu kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2022
Ujumbe wa Umoja wa Ulaya kuhusu uangalizi wa uchaguzi (EU EOM) nchini Kenya leo umewatuma waangalizi 48 katika kaunti 39 kati ya kaunti 47, ili kuanza uchunguzi wa muda mrefu wa uchaguzi mkuu wa tarehe 9 Agosti 2022.
Kufuatia mwaliko kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kenya, EU EOM, ikiongozwa na Mwangalizi Mkuu Ivan Štefanec, Mbunge wa Bunge la Ulaya kutoka Slovakia, ilianzisha shughuli zake jijini Nairobi tarehe 27 Juni baada ya kuwasili kwa kikundi kikuu cha wataalam 12.
Katika makao makuu ya EOM jijini Nairobi, Mwangalizi Mkuu alisema: “Leo tunayatuma makundi 24 ya Waangalizi wa Muda Mrefu, kila kikundi kikiwa na wajumbe wawili, ambao watatathmini vipengele kadhaa vya mchakato wa uchaguzi ikijumuisha kampeni na maandalizi ya uchaguzi kote nchini Kenya. Waangalizi wa Muda Mrefu wana umuhimu mkubwa katika kutathmini kwa kina mchakato wote wa uchaguzi kulingana na mbinu za Umoja wa Ulaya ya uangalizi wa uchaguzi”.
Waangalizi wa Muda Mrefu (LTOs) wanatoka katika mataifa 25 ya wanachama wa Umoja wa Ulaya, vile vile taifa la Norway na Uswizi. Watafanya mikutano na maafisa wa uchaguzi wa mitaa, wagombeaji, wawakilishi kutoka vyama vya kisiasa , pia mashirika ya kiraia na vyombo vya habari hadi, na baada ya siku ya uchaguzi. Taarifa itakayokusanywa itafahamisha kikundi kikuu cha EU EOM kilicho jijini Nairobi kuhusu mambo yanayojiri yanayohusiana na uchaguzi katika kaunti na maeneo bunge kote nchini.
Misheni itaimarishwa karibu na siku ya uchaguzi na Waangalizi 48 wa muda mfupi (STOs) na wajumbe kutoka Bunge la Ulaya. Wawakilishi zaidi wa balozi za EU vile vile balozi za Norway, Uswizi na Canada pia watajiunga na kikosi hiki.
EU EOM itawasilisha matokeo yake ya awali kwa umma muda mfupi baada ya siku ya uchaguzi (Agosti 9) na itasalia nchini Kenya hadi kukamilika kwa hatua zote za mchakato wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kurudiwa kwa uchaguzi wa urais, na mchakato wa malalamiko na rufaa. Ripoti ya mwisho ambayo itajumuisha mapendekezo itachapishwa takriban miezi mitatu baada ya uchaguzi kukamilika.
EU EOM inaongozwa na kanuni za maadili, ambazo zinahakikisha kutoegemea na kutopendelea upande wowote. Inafanya kazi yake kwa mujibu wa ‘Kanuni za Uangalizi wa Uchaguzi wa Kimataifa’ zilizoidhinishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2005.
EU EOM inatekeleza majukumu yake tofauti kabisa na wajumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Kenya na ni huru katika kutoa matokeo yake kutoka nchi wanachama wa EU, na taasisi zote za EU.
Kwa habari zaidi, tafadhali wasiliana na maafisa wa habari wa EU EOM Kenya 2022.
Marek Mracka,
Afisa wa Habari
marek.mracka@eomkenya2022.eu
+254 712 07 09 07
Faith Wamalwa
Afisa msaidizi wa habari
faith.wamalwa@eomkenya2022.eu
+254 728 66 94 62