“Chumvi haina ladha, sukari si tamu.”
Uvamizi wa Urusi katika maeneo ya mashariki mwa Ukraine ulianza katika mwaka wa 2014. Katika kipindi hiki, Warusi wamejaribu kuondoa kila kitu cha Kiukraine katika nyanja zote za maisha, na sekta ya chakula haijaachwa nyuma. Sasa, badala ya bidhaa za Kiukraine, bidhaa za Urusi au zilizoagizwa kutoka nchi “zinazoichukulia Urusi kwa urafiki” zinapatikana kwenye vibanda vya masoko na rafu za maduka makubwa. Watu hulalamika kuhusu uduni wake na kutamani bidhaa zao wanazozipenda kutoka kwa wazalishaji wa Kiukraine, lakini hawana chaguo kubwa.
Soma zaidi ili kufahamu jinsi maisha yalivyobadilika katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa muda wa Urusi (TOT), kupitia simulizi za watu waliokulia huko.
“Warusi walighushi kila kitu”: Hadithi kutoka Luhansk
Kwa watu wengi wanaoishi chini ya uvamizi, bidhaa za Kiukraine zimekuwa ishara ya maisha ya amani — kipindi ambacho hakukuwa na vita wala vikwazo, na rafu za maduka makubwa zilikuwa zimejaa bidhaa.
“Maandishi kwenye lebo na mabango ya maduka yalibadilika, na minyororo ya maduka ya Urusi ikachukua nafasi ya mitandao mikubwa ya maduka ya Kiukraine. Ghafla, kila kitu kilichotuzunguka kikawa cha kigeni. Ilikuwa kana kwamba ulilala nyumbani kwako na ukaamka katika nchi nyingine. Kwa upande mmoja, huenda jambo hili likaonekana kuwa ndogo. Je, kuna tofauti gani kuhusu aina ya mafuta ya alizeti utakayotumia au chokoleti utakayokula? Lakini kwa kweli, mambo haya yote huathiri jinsi unavyouona ulimwengu unaokuzunguka.
Ukienda Italia, unanunua chakula katika maduka yenye mabango yaliyoandikwa kwa Kiitalia, na bidhaa zina lebo zilizoandikwa kwa Kiitalia. Ukienda Ujerumani au, tuseme, Denmaki — ni vivyo hivyo. Kuna msemo usemao: “Wewe ni kile unachokula.” Tulipojikuta tukiishi chini ya uvamizi, msemo huu ulipata maana mpya,’ anasema Eva (si jina lake halisi, limebadilishwa kwa sababu za usalama), anayeishi Luhansk iliyovamiwa na Urusi.
Kulingana naye, bidhaa bandia zenye ubora duni hujitokeza madukani mara kwa mara. Wazalishaji wa Urusi hughushi lebo na kutumia majina ya chapa za biashara za Kiukraine ili kuongeza mauzo na kuwapa watu hisia kwamba hawajapoteza chochote.
‘Walighushi kila kitu: maziwa yaliyokolezwa, vinywaji baridi, maji ya madini, peremende, na hata chumvi. Lakini ubora si ule uliokuwepo kabla ya uvamizi, wala ladha si ile ile. Husababisha karaha tu,’ Eva anahitimisha.
Anaongeza kuwa kila alipofanikiwa kusafiri hadi katika eneo linalodhibitiwa na serikali ya Ukraine, alikimbia mara moja kununua ‘Zhyvchyk’ — kinywaji maarufu cha Kiukraine.
‘Hii ndiyo ladha ya utoto wangu, ya siku zisizo na wasiwasi, ambayo hunijaza kumbukumbu na kunihakikishia kwamba kila kitu kiko sawa,’ anasema.
Sehemu ya Oblast ya Luhansk ilivamiwa katika mwaka wa 2014. Katika kipindi hiki cha miaka minane (2014–2022), watu kutoka wilaya zilizovamiwa walivuka kituo cha ukaguzi cha Stanytsia Luhanska ili kununua bidhaa za Kiukraine. Vita vya uvamizi kamili vilipoanza, urusi iliteka karibu eneo lote. Wakazi wa eneo hilo walikimbia vita kwa wingi, wakiacha biashara zao nyuma, huku minyororo mikubwa ya maduka ikitangaza kufunga maduka yao. Katika miji ambako mapigano makali yalitokea, uporaji uliongezeka.
Hali ilipotulia, Warusi na washirika wao wa eneo hilo walianza kutwaa biashara, majengo ya kibiashara na kila kitu walichoweza kukipata, huku wakiwaambia wamiliki halisi kwamba sasa wao ndio ‘watawala’ wapya.
Mahitaji huamua usambazaji. Katika miji iliyopoteza si tu miundombinu yake bali pia sehemu kubwa ya wakazi wake, mikahawa ya gharama kubwa na maduka makubwa yakawa hayana maana tena.
Katika Rubizhne, ambako kabla ya uvamizi kulikuwa na maduka makubwa sita na makumi ya mikahawa, sasa kuna duka moja tu linalofanya kazi likiwa na bidhaa chache zaidi, pamoja na maeneo machache ya kula ambayo yanahudumia sanasana wanajeshi wa Urusi. Tofauti na wakazi wa eneo hilo, wao wana uwezo wa kifedha wa kununua. Baadhi ya maduka ya vyakula na maduka ya dawa yamegeuzwa kabisa kuwa maduka ya vifaa vya kijeshi.
Ladha iliyotoweka: Hadithi kutoka Horlivka
Ivan Frolov, mpiga picha kutoka Horlivka, anakumbuka jinsi kila kitu kilivyokuwa kikibadilika. Mwanzoni mwa kipindi cha 2014–2015, bidhaa za Kiukraine zilikaribia kutoweka kabisa kwenye rafu za maduka — kwanza, bidhaa zilizokuwa zimebaki ziliuzwa, kisha usambazaji wa bidhaa mpya ukasitishwa. Badala yake, bidhaa za Urusi zilianza kuonekana. Katika baadhi ya viwanda vilivyokuwa katika maeneo yaliyotekwa, mashine zilezile na hata baadhi ya taratibu zilibaki, lakini ladha haikuwa ile ile.
‘Hata hivyo, wazalishaji wa ndani na wakulima wa eneo hilo walikuwa bado ni wale wale; Urusi haikuwabadilisha,’ anakumbuka.
Kitu ambacho watu walikikosa zaidi ni peremende, vitafunwa, juisi na bidhaa za maziwa zilizotengenezwa nchini Ukraine. Bidhaa zilizoagizwa kutoka Urusi zilipoanza kuonekana kwenye rafu, tofauti ilionekana mara moja.
Wakati huo, Ivan hakufikiria kuhusu bei kwa sababu alikuwa mtoto. Lakini anakumbuka familia yao ikiishi maisha ya kawaida. Walikuwa na pesa za kutosha kununua bidhaa za msingi; mara nyingine waliweza kujinunulia kitu kitamu — kwa kawaida sokoni au katika duka la eneo hilo.
Pia, hakukuwa na bidhaa nyingi za kuchagua. Kila mara mvulana huyo alishangazwa na jinsi bidhaa zilizokuwa zinapatikana katika maduka makubwa ya ‘ATB’ au ‘Silpo’ katika maeneo yasiyokuwa chini ya uvamizi nchini Ukraine zilivyokuwa nyingi na zenye kuvutia zaidi. Huko Horlivka, mji wao wa nyumbani, hali hiyo ilitoweka.
‘Bado kulikuwa na uhaba; nilitaka kitu kipya, kitamu na cha aina mbalimbali,’ anaongeza.
Maksym Frolov, kaka yake Ivan, alikuwa mkubwa zaidi wakati wa uvamizi — alikuwa amefikia miaka 16 wakati huo, hivyo alikumbuka maelezo vizuri zaidi.
Mwanzoni mwa mwaka wa 2014, bidhaa za Kiukraine bado zilipatikana, lakini zilikuwa zikipungua siku baada ya siku. Baadaye, mapigano yalipotulia kwa muda, bidhaa za Urusi zilianza kuonekana kwenye rafu. Maksym aliziona kwa mara ya kwanza katika majira ya mchipuko. Karibu Aprili au Mei, pia aliona ruble za Urusi kwa mara ya kwanza.
‘Ilisikitisha kuona kila kitu cha Kiukraine kikitoweka taratibu,’ anakumbuka kijana huyo.
Vita vilisimama, lakini pamoja navyo, hali ya maisha nayo ilitoweka — mji ukaacha kufanya kazi.
Kitu ambacho Maksym alikikosa zaidi ni peremende za Kiukraine, crisps nzuri na juisi. Alikuwa amepata muda wa kuonja bidhaa hizo kidogo kabla ya uvamizi.
Lakini suala halikuwa tu kuhusu bidhaa. Maduka yaliyokuwa yakijulikana kama ‘ATB’, ‘Amstor’, na ‘Furshet’ yalitoweka. Yalifungwa au yaliendelea kufanya kazi bila kutambuliwa rasmi. ‘Nilikosa ukubwa wa huduma na kiwango cha maisha tulichozoea,’ anaeleza kijana huyo aliyelazimika kuhama makazi.
Maksym alipoondoka TOT kwa mara ya kwanza — kwanza akaenda Bakhmut, kisha Toretsk na baadaye Kyiv — alikuwa akitembea tu kwenye maduka na kuangalia bidhaa zilizokuwa zinauzwa.
Pia alikumbuka mazungumzo fulani. Mahali fulani karibu na Debaltseve, alisikia wanaume wazee wakiwa kwenye foleni na wakijadili bidhaa walizohitaji kuleta. Mmoja wao alisema: “Chumvi haina ladha, sukari si tamu.” Maksym alikumbuka sentensi hiyo milele. ‘Kwa kifupi, inaeleza kabisa kiwango cha ubora wa bidhaa za Urusi,’ anasema.
Maksym anaongea waziwazi kuhusu pesa. Alisikia simulizi kutoka kwa watu aliowafahamu ambao walifanya kazi chini ya uvamizi. Mmoja wao aliyefanya kazi katika kiwanda cha mikate alifanya kazi kwa zamu za saa 12 kuanzia saa 5 am, akipata takriban ruble 7,000 kwa mwezi — karibu UAH 2,500 (EUR 100) wakati huo. Wengine waliofanya kazi katika huduma za umma walipata hata pesa chache zaidi, takriban ruble 3,000 (EUR 45). “Ndivyo hali ilivyokuwa: “Kula makaroni yaliyopikwa kwa maji ya bomba,’’ alisikia kutoka kwa rafiki yake na akakumbuka.
Bei chini ya uvamizi zilikuwa karibu sawa na zile za Ukraine, lakini watu hawakuwa na pesa. Maksym anakumbuka jinsi fedha taslimu zilivyoletwa kutoka Ukraine na hryvnia kubadilishwa kuwa ruble, lakini pesa hizo zilitosha tu kuendesha maisha.
Hata hivyo, baadhi ya bidhaa zilibaki. Kwa mfano, bia ya ‘Sarmat’. Kiwanda cha kutengeneza bia huko Donetsk kiliendelea kufanya kazi, ila jina lake lilibadilishwa. Kutoka Luhansk, watu wakati mwingine walileta ‘Makdak’ — vitafunwa vya mahindi alivyokuwa anapenda alipokuwa mtoto.
Propaganda ya Urusi huunda taswira kwamba kila kitu katika maeneo yaliyovamiwa na Urusi kiko “kama zamani tu.” Lakini yeyote aliyeishi huko anajua: ladha ya maisha iliyotoweka haiwezi kurejeshwa.