Jinsi vita vilivyoharibu michezo mashariki mwa Ukraine

Hadi hivi karibuni, mashariki mwa Ukraine ilikuwa mojawapo ya vituo muhimu vya michezo nchini humo. Timu ya Shakhtar Donetsk ilikuwa ikishiriki mara kwa mara katika Ligi ya Mabingwa, Uwanja wa Donbas Arena uliandaa mechi za Euro 2012, na klabu za soka, mpira wa magongo ya barafu na mpira wa kikapu za eneo hilo zilishindana katika ngazi ya juu kabisa. Maelfu ya watoto walifanya mazoezi katika akademia za michezo, wakiota siku moja kucheza katika viwanja vikubwa.

Vita vya Urusi vilibadilisha kila kitu. Uvamizi, mapigano na uharibifu vililazimisha klabu kuhamia maeneo mengine au kusitisha shughuli kabisa. Viwanja na majengo ya michezo yaliharibiwa na kuacha kizazi kizima cha watoto bila fursa ya kufikia miundombinu ya michezo. Hivi ndivyo vita vilivyobadilisha michezo katika mikoa ya Donetsk na Luhansk, na kile kilichosalia katika mfumo wa michezo wenye nguvu uliokuwa mashariki mwa Ukraine.

Jiji la soka lisilo na soka

Image
How war destroyed sport in eastern Ukraine

Donetsk ilikuwa wakati mmoja jiji la waridi, fahari ya uchimbaji madini na soka. Katika mwaka wa 1936, Shakhtar, mojawapo ya klabu zilizotwaa mataji mengi zaidi mashariki mwa Ulaya, ilianzishwa hapa. Katika Euro 2012, uwanja wake wa kiwango cha juu wakati huo uliandaa mechi za timu kubwa za taifa kama Uingereza na Ufaransa, pamoja na maonesho ya Beyoncé na Rihanna.

Leo, yote hayo ni historia. Vita na uvamizi wa mwaka wa 2014 vilibadilisha Donetsk na maisha ya wakazi wake kiasi ambacho hakikutambulika tena. Uwanja ambao hapo awali uliweza kuchukua zaidi ya mashabiki 50,000 sasa hauna shughuli. Kwa kukosa matunzo yanayofaa, Donbas Arena inaendelea kuharibika taratibu, kama ilivyo kwa bustani inayoizunguka. Pamoja na klabu hiyo, mamia ya maelfu ya wakazi walikimbia, na sasa wametawanyika kote duniani.

‘Kwa familia yetu, Shakhtar ni zaidi ya klabu ya soka — ni kiungo chetu na nyumbani. Nilipokuwa mtoto, baba yangu alikuwa akinipeleka kutazama mechi za nyumbani. Mwanzoni, tulienda RSC Olimpiyskiy — uwanja wa zamani wa nyumbani wa Shakhtar — na baadaye kwenye Donbas Arena. Bado nakumbuka nilivyohisi nilipoingia kwa mara ya kwanza kwenye uwanja huo mpya. Ilikuwa ya kuvutia sana kiasi kwamba bado nahisi msisimko nikifikiria tu kuihusu,’ anakumbuka Ihor, mzaliwa wa Donetsk aliyelazimika kuondoka jijini humo kutokana na vita vya mwaka wa 2014.

FC Shakhtar Donetsk ilipata umaarufu duniani kama mojawapo ya klabu bora zaidi barani Ulaya katika kukuza vipaji vya soka. Mkakati wa muda mrefu wa klabu hiyo ulilenga kusajili wachezaji wadogo na kurahisisha mchakato wao wa kuingia katika soka la Ulaya. Mbinu hiyo ilifanikiwa: klabu ilipata mamia ya mamilioni ya euro huku ikiutambulisha ulimwengu kwa wachezaji hodari kama Fred, Alex Teixeira, Douglas Costa, Fernandinho, Willian na wengine. Katika mwaka wa 2009, timu hiyo ilitwaa Kombe la UEFA baada ya kuifunga Werder Bremen mabao 2–1 katika fainali ya kihistoria — ushindi ambao kwa kiasi kikubwa uliwezeshwa na wachezaji wake kutoka Brazil.

Hata hivyo, wachezaji wa kigeni walikuwa sehemu tu ya hadithi hiyo. Hadi mwaka wa 2014, akademia ya vijana ya Shakhtar ilikuwa katika kituo cha kisasa sana cha mazoezi cha Kirsha mjini Donetsk. Baada ya vita kuanza, klabu ilibadilisha mfumo wake wa mazoezi. Kwa sasa, vijana hufanya mazoezi hasa katika Mkoa wa Kyiv. Kirsha iliharibiwa kwa mashambulizi ya makombora na kuporwa.

Mykhailo Mudryk wa timu ya Chelsea, Heorhiy Sudakov na Anatoliy Trubin wa Benfica, nguli wa muda mrefu wa safu ya ulinzi Mykola Matviyenko, na gwiji wa soka la Ukraine Yaroslav Rakitskyi wote ni wahitimu wa akademia ya Shakhtar.

Donetsk sasa imekuwa chini ya uvamizi wa Urusi kwa miaka 12. Mtu anaweza tu kukisia ni watoto wangapi walionyimwa fursa ya kujijengea jina katika soka katika kipindi hicho.

Wakati huohuo, nchi ya Urusi imejaribu kujinyakulia historia ya michezo ya jiji hilo. Katika mwaka wa 2020, klabu bandia yenye jina na nembo ya Shakhtar ilianzishwa katika Donetsk iliyovamiwa na Urusi, na baadaye ikaingizwa katika mfumo wa soka wa Urusi.

Zaidi ya soka

Soka ni sura moja tu ya urithi wa michezo wa Mkoa wa Donetsk iliyoharibiwa na vita. Katika mwaka wa 2014, ukumbi mkuu wa mpira wa magongo ya barafu na mpira wa kikapu wa Donetsk — Druzhba Arena — uliporwa na kuchomwa, na baadaye ukapata uharibifu zaidi.

Maeneo mengine kadhaa yalipata hatima kama hiyo. Mojawapo ya majengo makubwa zaidi ya michezo ya ndani nchini Ukraine, Illichivets mjini Mariupol, Altair Ice Arena mjini Druzhkivka, Donbas Equicentre mjini Donetsk, Kramatorsk Sports Complex, Volodymyr Boyko Stadium mjini Mariupol, na Metalurh Stadium mjini Bakhmut, yote yaliharibiwa au yaliacha kabisa kufanya kazi kutokana na vita.

Pamoja na miundombinu ya michezo, vita pia vilibadilisha hatima ya klabu za kitaaluma. Baadhi zilitoweka kabisa, huku nyingine zikipoteza hadhi yao ya kitaaluma au kulazimika kuondoka katika miji yao ya nyumbani na kucheza kwa miaka mingi mbali na mashabiki’ wao.

Mkoa wa Luhansk ukikabiliwa na hatima hiyo hiyo

Katika Mkoa wa Luhansk, ambao karibu wote umavamiwa na Urusi, hali si nzuri zaidi. Kama Donetsk, timu kubwa ya soka ya mkoa huo, Zorya Luhansk, ililazimika kuondoka katika jiji lake la nyumbani kutokana na vita. Klabu hiyo haikuweza kusherehekea miaka 100 tangu kuanzishwa kwake katika uwanja wake wa nyumbani, Avanhard Stadium.

Katika maeneo yaliyotekwa, mamlaka za Urusi zilianzisha klabu bandia yenye jina hilo hilo na kuiingiza katika mfumo wao wa soka. Uwanja wa Avanhard wa timu ya Luhansk, ambao hapo awali ulikuwa uwanja wa nyumbani wa Zorya halisi, sasa umechakaa. Kwa kukosa matengenezo ya kutosha, miundombinu yake inaendelea kuzorota taratibu, na uwanja wenyewe hutumiwa zaidi kwa mashindano ya ndani na matukio yanayounga mkono mamlaka za uvamizi wa Urusi.

Ingawa Zorya iliweza kunusurika baada ya kulazimika kuhama, klabu nyingine maarufu ya Mkoa wa Luhansk ilifungwa.

Katika mwaka wa 2015, baada ya jitihada zisizofanikiwa za kuihifadhi timu huku jiji likiwa chini ya uvamizi, FC Stal Alchevsk ilijiondoa katika Ligi ya Kwanza na kuvunjwa. Baadaye, vikosi vya uvamizi vilianzisha klabu iitwayo Metalurh huko Alchevsk ili kushiriki katika mashindano yaliyoandaliwa na Urusi, ikitumikia madhumuni ya propaganda badala ya michezo.

Miundombinu ya michezo katika miji mingine ya Mkoa wa Luhansk pia imeathirika pakubwa. Jumba la Michezo ya Barafu la Sievierodonetsk, Jumba la Michezo la Olymp mjini Kreminna, Jumba la Michezo la Budivelnyk na Uwanja wa Shakhtar mjini Lysychansk, pamoja na kumbi za michezo za eneo hilo na akademia za vijana, zimeharibiwa, kuathiriwa au kuachwa.

Nyuma ya kila moja ya majengo haya kuna simulizi binafsi za watu ambao michezo ilikuwa sehemu muhimu ya maisha yao.

Kizazi kilichopoteza fursa

Vita viliiba mambo mengi zaidi ya viwanja na klabu kutoka mashariki mwa Ukraine. Maelfu ya watoto walipoteza fursa ya kufanya mazoezi, kukuza vipaji na kufuatilia mustakabali katika michezo. Hivi leo, haiwezekani kuhesabu ni wachezaji wangapi watarajiwa wa soka, mpira wa kikapu, riadha au mabingwa wa baadaye wa Olimpiki walinyimwa fursa yao kutokana na uvamizi na vita. Viwanja vilivyoharibiwa vinaweza kujengwa upya, lakini miaka ya utoto iliyopotea haiwezi kurejeshwa.

Hata hivyo, ustahimilivu wa Shakhtar na Zorya unaonyesha kwamba uvamizi hauwezi kufuta historia na utambulisho. Bila viwanja vyao vya nyumbani, klabu halisi za Ukraine zinaendelea kuwepo, zikiwakilisha miji yao kutoka mbali, huku klabu bandia zilizoanzishwa na wavamizi zikiwa majaribio yasiyo na mafanikio ya kujinyakulia urithi wa mtu mwingine.

Michezo katika Mikoa ya Donetsk na Luhansk inakabiliwa na kipindi chake kigumu zaidi. Hata hivyo, kumbukumbu za viwanja vilivyojaa mashabiki na ushindi wa kihistoria bado zinaendelea kuishi — pamoja na matumaini kwamba siku moja michezo ya kiwango cha juu itarejea nyumbani.