Upungufu wa Taarifa
Kwa usiri mkubwa na kwa kutumia mtandao binafsi wa faragha, watoto wa Ukraine huingia kwenye madarasa ya mtandaoni. Wengine husubiri hadi usiku wa manane, wakati vizuizi vya intaneti vinapolegezwa, wakitumai kutuma kazi zao walizokamilisha kwa walimu walioko katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali ya Ukraine. Wanajua kwamba kufanya hivyo ni hatari. Watoto wa Ukraine wakikamatwa wakishiriki katika masomo hayo, familia zao hukabiliwa na madhara makubwa. Jambo mbaya zaidi ni kwamba kudumisha uhusiano huo kunazidi kuwa vigumu. Tangu Urusi ilipoanza kutawala Crimea na sehemu za mikoa ya Donetsk na Luhansk katika mwaka wa 2014, upatikanaji wa vyombo vya habari na elimu ya Ukraine umekuwa ukizidi kuwa mgumu. Ilianza kwa kuzuiwa kwa tovuti. Sasa hali hiyo imebadilika na kuwa mazingira ya taarifa yanayodhibitiwa kwa ukali, ambapo vyombo vya habari huru haviwezi kufikiwa, majukwaa ya mawasiliano yamewekewa vikwazo, na hata kuwa na baadhi ya programu kwenye simu au vifaa vingine kunaweza kuwafanya watu washukiwe.
Kulingana na Kateryna Rashevska, mwanasheria wa kimataifa na mtaalamu katika Kituo cha Kikanda cha Haki za Binadamu, Urusi imeongeza kwa kiwango kikubwa juhudi zake za kudhibiti upatikanaji wa taarifa kwa Waukraine katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
"Shirikisho la Urusi, hasa kuanzia mwaka wa 2025, ingawa hatua zilianza kuchukuliwa kabla ya hapo, limepitisha sera ya kufunga kabisa upatikanaji wa taarifa kwa sababu hatua hiyo huliruhusu kudhibiti kikamilifu fikra za kizazi cha vijana," anasema.
Anarejelea kauli ya Rais wa Urusi, Vladimir Putin wakati wa mkutano na washiriki wa kile kinachoitwa "operesheni maalumu ya kijeshi."
"Leo mstari wa mbele wa mapambano uko katika fikra za kizazi cha vijana, na katika uwanja huo wa mapambano Urusi ina wajibu wa kushinda."
Kwa Rashevska, maneno hayo yanaeleza kwa nini taarifa zimegeuka kuwa uwanja mwingine wa vita.
Baada ya kuzuia tovuti za Ukraine, Urusi imeweka vikwazo vya kisheria pamoja na mbinu za vitisho zinazolenga kuwazuia watu kupata taarifa huru. Anasema kuw familia hukabiliwa na adhabu ikiwa vyombo vya usalama vya Urusi vitagundua programu zilizopigwa marufuku au mawasiliano yasiyoruhusiwa wakati wa ukaguzi wa simu.
"Kuna udanganyifu na wakati mwingine vitisho vya moja kwa moja... ikiwa wakati wa ukaguzi wa simu za mkononi, kipktlishi au tableti zitapatikana kuwa na programu zilizopigwa marufuku, kama vile Zoom, Telegram au WhatsApp, basi familia nzima inaweza kupata matatizo, pamoja na mtoto."
Anaongeza kuwa baadhi ya familia zilizojaribu kuondoka katika maeneo yaliyomilikiwa zimeshutumiwa kwa uhaini baada ya maafisa kugundua mawasiliano yao na mamlaka za Ukraine kwenye vifaa vyao.
Vizuizi vinavyozidi kuimarishwa pia vinabadilisha upatikanaji wa elimu ya Ukraine.
Kulingana na Wizara ya Elimu na Sayansi ya Ukraine, takriban watoto 44,000 waliokuwa wakiishi katika maeneo yaliyotekwa walikuwa wamejisajili katika masomo ya mtandaoni ya Ukraine katika mwaka wa 2024. Kufikia mwisho wa mwaka wa 2025, idadi hiyo ilikuwa imeshuka hadi kati ya watoto 32,000 na 33,000. Rashevska anaonya kuwa takwimu hizi huenda zikawa ndogo kuliko hali halisi, kwa sababu watoto wengi hutumia huduma za VPN zinazoficha mahali walipo.
"Hatujui leo ni watoto wangapi bado wanaendelea kudumisha uhusiano huu na Ukraine kupitia elimu," anasema. "Elimu haihusu kupata maarifa, kujenga utu na kukuza maendeleo pekee, inahusu pia kuhifadhi utambulisho wa mtu na kudumisha uhusiano wake na nchi yake."
Mamlaka za Urusi zinawataka watoto kuhudhuria shule zilizoanzishwa katika maeneo yaliyotekwa, na hivyo kufanya elimu ya Urusi kuwa ya lazima huku zikiondoa elimu inayotolewa kwa lugha ya Kiukraine. Mtaala wa Urusi umejaa maudhui ya kijeshi na propaganda zinazounga mkono vita. Kwa watoto wanaolazimika kuhudhuria shule hizo, kuna nafasi ndogo sana ya kuendelea na masomo yao ya Kiukraine. Hata hivyo, wazazi wanaokataa kuwapeleka watoto wao katika shule za Urusi wako katika hatari ya kushtakiwa kwa mujibu wa sheria za Urusi.
Vizuizi hivyo haviishii darasani pekee.
Andrii Dikhtiarenko, mwanzilishi na mhariri mkuu wa gazeti la Realna Hazeta, ambaye anatoka katika mkoa wa Luhansk, ametumia miaka mingi kurekodi na kuripoti maisha ndani ya maeneo yaliyotekwa.
"Kuanzia mwaka 2014, vikosi vya uvamizi vilianza hatua kwa hatua kuzuia upatikanaji wa vyanzo mbalimbali vya taarifa. Haya yote yalianza takriban mwaka wa 2015–2016, wakati watoa huduma za intaneti wa eneo hilo walipolazimishwa na kile kinachoitwa Wizara ya Habari, FSB na vyombo vyake vya usalama vinavyofanya kazi kwa niaba yake, kuzuia upatikanaji wa tovuti nyingi za habari kutoka Ukraine na maeneo mengine."
Chumba chake cha habari kilikuwa miongoni mwa vilivyofungiwa.
Wakazi walijifunza haraka kukabiliana na hali hiyo kwa kutumia huduma za VPN kuvunja vizuizi hivyo. Lakini kadiri Urusi ilivyozidi kuimarisha udhibiti wake, orodha ya majukwaa yaliyopigwa marufuku iliongezeka na kujumuisha mitandao ya kijamii, huduma za mawasiliano na programu zilizokuwa zikitumika kuwasiliana na ndugu walio nje ya maeneo yaliyotekwa.
"Sasa kuna uwezekano wa kutumia VPN, jambo ambalo pia lina hatari kubwa, au kutumia huduma nyingine za mawasiliano ambazo bado hazijazuiwa."
Anaeleza kuwa hata njia hizo bado hazina uhakika, kwa sababu hali ya vizuizi hubadilika mara kwa mara. Kwa wanahabari, kuwafikia wasomaji na watazamaji walioko katika maeneo yaliyotekwa kunahitaji kuendelea kubadilisha mbinu na kutafuta mbinu mpya kila wakati.
Baada ya majukwaa kama Facebook na YouTube kuwa magumu zaidi kufikiwa, Realna Hazeta imehamishia sehemu kubwa ya shughuli zake kwenye TikTok.
"Takriban asilimia 30 hadi 40 ya watazamaji wetu wa TikTok bado wanatoka katika maeneo yaliyotekwa. Tumehesabu hilo."
Ingawa anaamini kuwa wakazi wengi vijana wamejifunza kutumia VPN na kutafuta vyanzo mbadala vya taarifa, anasema hakuna takwimu za kuaminika zinazoonyesha ni watu wangapi wanaoendelea kupata taarifa kutoka kwa vyombo huru vya habari, hasa miongoni mwa watu wa vizazi vya zamani wenye ujuzi mdogo wa matumizi ya teknolojia za kidijitali.
Mawasiliano yenyewe yamekuwa jambo hatari.
Watu mara nyingi hutegemea simu za sauti kupitia Telegram, barua pepe au programu nyingine za mawasiliano ambazo hazijawekewa vikwazo vikali. Wamelazimika kubadili namna wanavyowasiliana, wakijikita zaidi katika mazungumzo ya kawaida, kwa sababu mamlaka za Urusi zinaweza kukagua simu kwa urahisi.
"Watu wanaweza kusimamishwa na kuagizwa kufungua simu zao. Wanachunguza mawasiliano yao, wanafuatilia watu wanaowasiliana nao na chaneli za Telegram walizojiunga nazo."
Mazungumzo ya kisiasa na jamaa kwa kiasi kikubwa huepukwa.
"Tunawasiliana na jamaa zetu hasa kuhusu masuala ya kila siku yanayohusiana na maisha na kujikimu, na pia tunajitahidi kuepuka kuzungumza mambo ya siasa."
Anasema kuwa vyombo vya habari vinavyodhibitiwa na Urusi vinaendeleza mazingira ya ukandamizaji kwa kutoripoti matatizo yanayowakabili wakazi wa maeneo hayo, huku vikisukuma simulizi zinazodai kuwa maeneo hayo yatastawi chini ya utawala wa Urusi.
"Havizungumzii matatizo yanayowakabili watu. Badala yake, vinaendelea kusema kwamba maeneo yaliyotekwa yanakaribia kustawi chini ya utawala wa Urusi... Upungufu halisi wa taarifa umetengenezwa."
Kwa Rashevska, athari zake zinaenda mbali zaidi ya vita vyenyewe.
Akirejelea tafiti kuhusu athari za muda mrefu za kuwalazimisha watu kuacha utambulisho wao na kujiunga na utamaduni mwingine, anaonya kwamba kutengwa kwa muda mrefu, kufundishwa itikadi za propaganda na kuingizwa katika utamaduni wa kijeshi kunaweza kuwaacha watoto wanaokulia katika maeneo yanayokaliwa na majeraha ya kudumu ya kisaikolojia.
"Watoto hawa, na hasa vijana, watahitaji huduma maalumu, huduma maalumu za kijamii, usaidizi wa kurekebisha afya ya akili na huduma za kuwawezesha kujumuika tena katika jamii ili waweze kurejea kwenye maisha ya kawaida."
Katika maeneo ya Ukraine yaliyotekwa, upatikanaji wa taarifa si suala la kuwa na muunganisho wa intaneti pekee tena. Umekuwa mapambano ya kulinda utambulisho, kumbukumbu na uwezo wa kizazi kizima kuendelea kuunganishwa na nchi ambayo bado wanaiita nyumbani.