Tamko la Pamoja kutoka Ubalozi wa Uingereza, Canada, Norway, Uswisi, Ubelgiji, Denmark, Ufini, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Poland, Slovakia, Hispania, Uswidi, na Ujumbe wa Umoja wa Ulaya kuhusu Matukio ya Hivi Karibuni Nchini Tanzania

Tunarejea tamko la Mwakilishi Mkuu kwa niaba ya Umoja wa Ulaya la tarehe 2 Novemba 2025, na tamko la pamoja la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Norway na Uingereza la tarehe 31 Oktoba 2025, kuhusu uchaguzi nchini Tanzania.


Tumehuzunishwa sana kwa vifo na majeruhi wengi waliotokana na matukio ya wakati wa uchaguzi.


Tunatambua azma ya serikali ya kudumisha amani na utulivu wa nchi, na tunasisitiza umuhim wa vyombo vya ulinzi kutekeleza majukumu yao kwa uangalifu mkubwa. Tunarudia wito wetu kwa serikali kutekeleza ahadi zake za kimataifa za kulinda haki za msingi, ikiwemo, haki za kikatiba za kupata taarifa na uhuru wa kujieleza kwa Watanzania wote.

Taarifa za kuaminika kutoka mashirika ya kitaifa na kimataifa zinaonesha ushahidi wa mauaji nje ya utaratibu wa kisheria, kupotea kwa watu, ukamataji wa wetu kiholela na ufichaji wa mili ya waliopoteza maisha. Tunatoa wito kwa mamlaka husika kukabidhi mili ya marehemu kwa familia zao haraka iwezekanavyo, kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa na kuhakikisha waliokamatwa wanapata misaada ya kisheria na matibabu. Zaidi, tunatoa wito kwa serikali kushughulikia mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti za awali za waangalizi wa uchaguzi wa AU na SADC ambazo ziliweka bayana mapungufu yaliyojiri wakati wa mchakato wa uchaguzi.

Tunakaribisha hatua ya Serikali ya kutambua kwamba kuelewa kiini na mazingira yaliyopelekea vurugu, ikiwemo vifo, ni hatua muhim kuelekea upatikanaji wa haki na maridhiano. Uchunguzi wowote lazima uwe huru, wazi na shirikishi - ukijumuisha asasi za kiraia, taasisi za kidini, na wadau wote wa kisiasa.